Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, katika siku ya kwanza ya muongo mtukufu wa Fajr, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika mkutano na maelfu ya watu kutoka tabaka mbalimbali za wananchi, aliitaja tarehe 12 Bahman kuwa ni siku ya kipekee na ya kihistoria. Akirejea mabadiliko ya utawala wa Pahlavi kutoka kwenye mfumo wa “mtu mmoja, wa kidikteta, usio wa kidini na tegemezi” kwenda kwenye utawala “wa wananchi, unaotegemea dini na unaosimama dhidi ya uonevu wa madola makubwa”, alisema: Wananchi waliigeuza kuwa majivu fitna ya hivi karibuni ya Kimarekani-Kizayuni, kama walivyofanya kwa njama zote za awali, na katika siku zijazo pia, taifa hili kwa uongozi wa Mwenyezi Mungu, litakabiliana na tukio lolote na kulimaliza kabisa.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei pia alitaja juhudi za Marekani za kuitafuna Iran na msimamo thabiti wa taifa shupavu la Iran dhidi ya tamaa hiyo kuwa ndio chanzo kikuu cha uhasama wa miaka 47 kati ya Iran na Marekani. Akirejea kauli za hivi karibuni za Wamarekani, aliongeza kuwa: Wao hapo awali pia walikuwa wakisema kwa lengo la kulitisha taifa la Iran kwamba “chaguo zote ziko mezani”, na wajue kwamba iwapo safari hii wataanzisha vita, vita hivyo vitakuwa vita vya kikanda.
Katika mwanzo wa hotuba yake, akirejea mapokezi ya kipekee na ya umoja mkubwa ya wananchi kwa Imam Khomeini (rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) tarehe 12 Bahman 1357, alisema: Imam, licha ya vitisho vyote, aliingia Tehran kwa ujasiri na nguvu, na akayageuza mapokezi makubwa na ya ajabu ya wananchi kuwa msingi wa kuunda mfumo mpya, na siku hiyo hiyo ya kuwasili alitangaza kuanguka kwa utawala wa kifalme.
Kiongozi wa Mapinduzi alieleza kuwa; kubadilishwa kwa utawala wa mtu mmoja na wa kidikteta kwenda kwenye utawala ambao wananchi ndio wahusika wakuu, pamoja na kubadilishwa kwa mwelekeo usio wa kidini uliopigiwa debe na Pahlavi kuwa mwelekeo wa Kiislamu, ni sifa mbili kuu za mfumo uliochipuka kutokana na jihadi ya Imam na taifa. Aliongeza kuwa: Kama viongozi wote wangetimiza majukumu yao kikamilifu, serikali ingekuwa ya kidini kikamilifu, lakini kwa ujumla tumesonga mbele katika mchakato wa kidini na Kiislamu.
Ayatullah Khamenei aligusia kurejeshwa nchi kwa wamiliki wake halisi—yaani wananchi—na kukatwa mkono na ushawishi wa Marekani nchini Iran kuwa ni sifa nyingine ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, na akasema: Sifa hii iliikasirisha na kuihuzunisha Marekani, na tangu siku hiyo ikaingia katika uadui dhidi ya taifa na mfumo huu.
Katika kufafanua sura ya wananchi kuwa mhimili wa serikali, alirejea kuundwa kwa roho ya kujitegemea katika taifa na akasema: Imam mwenye hekima aliitambua jamii juu ya uwezo wake mkubwa na thamani zake, na akageuza kauli ya “hatuwezi” kuwa imani muhimu sana ya “tunaweza”.
Kiongozi wa Mapinduzi alieleza kuwa; matokeo ya sera, kujidharau na utegemezi wa enzi za Qajar na Pahlavi yalikuwa kugeuza taifa “kubwa lenye historia ang’avu ya ustaarabu na utamaduni” kuwa jamii “iliyodhalilishwa na iliyorudi nyuma”. Alisema: Katika kipindi hicho, katika nyanja za “sayansi na teknolojia, siasa, mtindo wa maisha, hadhi ya kimataifa, mizania ya kikanda” na maeneo mengine yote, tulikuwa tumebaki nyuma; lakini Imam Khomeini alivivia roho ya “kujiamini” ndani ya taifa na akabadili mwelekeo kwa nyuzi 180.
Ayatullah Khamenei akirejea maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali, aliongeza kuwa: Ni nani aliyedhani kuwa taifa la Iran lingefikia siku ambayo Wamarekani wangenakili silaha zilizotengenezwa na Iran? Haya yote ni matokeo ya kujiamini, matumaini na malengo ya juu ambayo Imam Khomeini, kama “kielelezo cha matumaini na kujitegemea”, aliyaingiza katika taifa na kuwahamasisha wananchi kufanya kazi na kusonga mbele.
Akikumbushia hila za mashetani wa nje na wa ndani wanaodai kuwa “kijana wa Kiirani hana matumaini wala mustakabali”, alisema: Kijana wa Kiirani ana matumaini, ana bidii, na mustakabali pia.
Kiongozi wa Mapinduzi aliitaja tarehe 22 Bahman kuwa ni siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na 12 Farvardin kiwa ni siku ya kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu kwa kura za wananchi, pamoja na maendeleo yote ya nchi, kuwa ni matunda ya siku tukufu ya 12 Bahman 1357, na akaongeza: Baraka za siku hii kuu zinaendelea kwa fadhila za Mwenyezi Mungu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, huku akisisitiza asili ya Marekani na Wazayuni ya “fitna ya tarehe 18 na 19 Dey”, aliwataja waharibifu kuwa wamegawanyika katika “viongozi wakuu” na “askari wa miguu”. Aliongeza kiwa: Viongozi wakuu, ambao wengi wao wamekamatwa, kama walivyokiri wenyewe, walipokea fedha kwa ajili ya vitendo vyao na walipata mafunzo ya jinsi ya kushambulia vituo na kuwakusanya na kuwahamasisha vijana; lakini kundi jingine la waharibifu lilikuwa vijana wenye jazba, ambao hatuna tatizo kubwa nao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alielezea kauli za rais wa Marekani kuwa ni dalili wazi ya kuwa fitna ya hivi karibuni ilikuwa ya Wamarekani na Wazayuni, na akasema: Yeye (Tump) waziwazi aliwaambia waharibifu aliowaita “wananchi wa Iran” kwamba: “Nendeni mbele, nami ninakuja!” Kwa mtazamo wao, maelfu haya machache ya waharibifu yalikuwa ndio wananchi wa Iran, lakini mamilioni ya watu waliokusanyika kote nchini tarehe 22 Dey hawahesabiwi kuwa wananchi wa Iran!
Ayatullah Khamenei alieleza kuwa fikra na njia mpya ya Jamhuri ya Kiislamu na msuguano wake na maslahi ya madhalimu wa dunia ndiyo sababu ya kuendelea kwa uadui wao, na akasema: Kwa sababu hiyo, fitna ya hivi karibuni haikuwa ya kwanza Tehran, wala haitakuwa ya mwisho, na huenda matukio kama haya yakajirudia pia katika siku zijazo.
Aliongeza: Uhasama huu utaendelea hadi pale ambapo taifa la Iran, kwa uthabiti, subira na udhibiti kamili wa mambo, litakapowakatisha tamaa maadui—na tutafikia hatua hiyo.
Akirejea matukio na uhalifu kama wa fitna ya hivi karibuni huko Tehran, mfano wa tarehe 30 Khordad 1360 ambapo wanafiki waliwashambulia basiiji kwa visu alisisitiza: Katika matukio yote haya, mkono wa wageni, hususan Marekani na utawala wa Kizayuni, unaonekana wazi.
Kiongozi wa Mapinduzi alisisitiza kuwa; katika fitna ya hivi karibuni na matukio ya miaka iliyopita, vyombo vya usalama, Basij, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (Sepah) na taasisi nyingine zilitimiza kikamilifu wajibu wao. Aliongeza: Lakini kilichozima moto wa fitna na kugeuza miale yake kuwa majivu—kama ilivyokuwa mwaka 2009—ni kuingia kwa wananchi uwanjani. Na baada ya hapa pia, iwapo tukio lolote litatokea kwa nchi, Mwenyezi Mungu atawainua wananchi hawa kukabiliana nalo, na wananchi watamaliza kazi.
Ayatullah Khamenei katika kufafanua sifa za fitna ya Kimarekani ya hivi karibuni, alitaja sifa ya kwanza kuwa ni kujificha kwa waharibifu nyuma ya maandamano ya wafanyabiashara, na akasema: Wapotoshaji, kama wahalifu wanaowatumia wanawake na watoto kama ngao wanaposhambulia miji, walijificha nyuma ya wafanyabiashara waliokuwa na madai ya kimantiki na halali na walitoka barabarani, ili wasitambulike.
Aliongeza kuwa: Hata hivyo, wafanyabiashara wenye busara walipoona vitendo vya waharibifu kama kushambulia vituo vya polisi badala ya maandamano ya amani, walijitenga nao na kuwaacha wapotoshaji peke yao.
Kiongozi wa Mapinduzi alitaja sifa ya pili ya fitna hiyo kuwa ni kuwa na sura ya mapinduzi ya kijeshi, na akasema: Fitna hii, kama ambavyo baadhi ya watu duniani pia walieleza, ilikuwa sawa na jaribio la mapinduzi ya kijeshi. Ingawa ilidhibitiwa, lakini uharibifu wa vituo nyeti na muhimu katika uendeshaji wa nchi kupitia mashambulizi dhidi ya polisi, vituo vya Sepah, baadhi ya taasisi za serikali na benki, pamoja na kushambulia vitu vitakatifu kama misikiti na Qur’ani, unaonesha ukweli huu.
Ayatullah Khamenei alisema; kubuniwa kwa fitna nje ya nchi na kuongozwa kwa viongozi wa ndani kwa kutumia nyenzo mbalimbali kama taarifa za satelaiti kuwa ni sifa nyingine ya ghasia za mwezi Dey, na akabainisha: Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa, afisa mmoja muhimu wa Kimarekani serikalini alimwambia mshirika wake wa Kiirani kwamba mashirika ya ujasusi ya CIA na Mossad yaliwekeza nguvu zao zote katika tukio hili.
Aliongeza kuwa; kuamriwa kwa viongozi waliopata mafunzo, kuuwa raia ilikuwa ni sifa nyingine ya ghasia hizo, na akasema: Kwa mujibu wa mpango huo, walishambulia vituo vya kijeshi na vya usalama kwa silaha binafsi za kisasa ili kwa majibu ya maafisa, watu kadhaa wafe; na kwa lengo la kuongeza idadi ya vifo, hata hawakuwaonea huruma askari wao waliowaleta uwanjani kwa propaganda, bali waliwalenga nao pia.
Kiongozi wa Mapinduzi, huku akielezea huzuni yake juu ya kufanikiwa kwa viongozi wa ghasia kuongeza idadi ya waliopoteza maisha, alisema: Moyo wa mtu unauma kwa ajili ya vijana hawa waliodanganywa na wasio makini.
Akirejea juhudi za adui kuonesha idadi ya waliouawa kuwa mara kumi zaidi, alisema: Walitaka idadi hiyo iwe kubwa zaidi; hata hivyo, idadi hii iliyopo pia inasikitisha sana.
Ayatullah Khamenei alitaja lengo kuu la adui kuwa ni kuvuruga usalama wa nchi, na akaongeza: Usalama unapokosekana, hakuna kitu—hakuna chakula, hakuna uzalishaji, hakuna biashara, hakuna masomo na utafiti, wala sayansi na maendeleo; kwa hiyo wale waliohifadhi usalama wa nchi wana deni la uhai juu ya shingo za wananchi wote.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza: Walitaka kuwaweka wananchi dhidi ya mfumo, lakini wananchi kwa mahudhurio yao ya mamilioni tarehe 22 Dey waliwapiga vibaya wenye nia mbaya na wakaonesha uhalisia wa taifa la Iran.
Akiwa amesisitiza kuwa viongozi lazima kwa dhati wawathamini wananchi hawa, alisema: Isitoshe, fitna hii, kwa bahati au kwa makusudi, ilifanyika katika kipindi ambacho serikali na viongozi walikuwa wanapanga sera na ramani ya kiuchumi ya nchi kwa ajili ya kuboresha hali.
Sifa ya mwisho aliyotaja Kiongozi wa Mapinduzi kuhusu fitna ya hivi karibuni ilikuwa ni vurugu zake za kidaesh.
Akirejea kukiri kwa rais wa sasa wa Marekani katika uchaguzi wake wa kwanza kuhusu kuhusika kwa serikali ya Marekani katika kuunda Daesh, alisema: Katika fitna ya hivi karibuni pia, Wamarekani waliwaunda Daesh ambao matendo yao yanafanana na Daesh yule yule. Daesh walikuwa wakiua watu kwa ukatili kwa kuwatuhumu ukafiri, na hawa pia waliwaangamiza watu kwa ukatili huohuo lakini kwa sababu ya dini; kwa unyama na ukatili wa ajabu waliwachoma watu wakiwa hai na wakawakata vichwa.
Ayatullah Khamenei katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake kuhusu sababu ya uadui wa zaidi ya miaka arobaini kati ya Marekani na Iran, alisema: Suala hili linaweza kufupishwa kwa maneno mawili: Marekani inataka kuimeza Iran, lakini taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu ni kizuizi; na kwa hakika kosa la taifa la Iran ni kwamba limeiambia Marekani, “una makosa makubwa” ukitaka kuimeza nchi yangu.
Alitaja vivutio vingi vya Iran kama mafuta, gesi, madini, pamoja na nafasi yake ya kimkakati na kijiografia kuwa vimechochea tamaa ya dola vamizi na yenye pupa kama Marekani, na akabainisha: Wao wanataka kuiteka Iran na kurejesha udhibiti wao juu ya rasilimali, mafuta, siasa, usalama na mahusiano ya kimataifa ya Iran kama ilivyokuwa wakati wa Pahlavi. Hiyo ndiyo sababu kuu ya uadui wao; kauli zao nyingine kama haki za binadamu ni porojo tupu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza: Taifa la Iran limesimama imara, limetua kifua chake mbele ya tamaa za Marekani, litasimama, na litawakatisha tamaa kutokana na hila na madhara yao.
Akirejea vitisho vya Wamarekani kuhusu vita na matumizi ya aina fulani za ndege, alisema: Kauli hizi si mpya; hapo zamani pia walikuwa wakitishia mara kwa mara kwamba chaguo zote ziko mezani; sasa pia mtu huyu anazidi kutoa madai ya aina hii, akisema tumeleta manowari.
Ayatullah Khamenei aliongeza: Taifa la Iran haliogopeshwi na mambo kama haya; haliguswi na kauli hizi. Sisi hatutakuwa waanzilishi wa vita, wala hatutaki kumdhulumu mtu au kuishambulia nchi yoyote; lakini taifa la Iran litampiga ngumi nzito yeyote atakayekuwa na tamaa, akataka kulishambulia au kulidhuru.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza tena: Wamarekani wajue kwamba iwapo safari hii wataanzisha vita, vita hivyo vitakuwa vita vya kikanda.
Maoni yako